Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ziyara hiyo, imelenga kumpongeza Dkt. Alhaji Sibtain pamoja na taasisi yake kutokana na juhudi na mchango wao katika kuwahudumia wananchi na kuchangia maendeleo ya kijamii.
Katika ziara hiyo, Sheikh Jalala amepongeza kwa dhati jitihada mbalimbali zinazofanywa na The Desk and Chair Foundation, hususan katika maeneo yanayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi. Miongoni mwa huduma hizo ni uchimbaji wa visima vya maji katika maeneo ya vijijini, utoaji wa madawati shuleni, pamoja na kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwapatia baiskeli ili kuwawezesha kujitegemea na kurahisisha shughuli zao za kila siku.
Akizungumza wakati wa ziyara hiyo, Sheikh Jalala alisisitiza umuhimu wa kujitolea katika kuwahudumia wanajamii, huku akirejea mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) yanayohimiza waumini kuwa na moyo wa kuwasaidia na kuwahudumia wengine.
Alieleza kuwa; kuwatumikia watu na kutatua changamoto zao ni miongoni mwa matendo mema yenye thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, hivyo juhudi za watu binafsi na taasisi katika kuwasaidia wenye mahitaji zinapaswa kuungwa mkono na kuhamasishwa.
Sheikh Jalala pia ameitumia fursa hiyo kumpongeza Dkt. Alhaji Sibtain kwa moyo wake wa kujitolea na kuendelea kuwekeza katika miradi yenye manufaa kwenye jamii, huku akisisitiza kuwa huduma hizo zina nafasi muhimu katika kuijenga jamii yenye mshikamano, utu na kujaliana.
Kwa upande wake, Dkt. Alhaji Sibtain amemshukuru kwa dhati Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge pamoja na msafara wake kwa kumtembelea, kumpongeza na kumpa moyo katika kuendelea na juhudi za kuitumikia jamii.
Amesema ziara hiyo ni ishara ya upendo, mshikamano na kuthamini juhudi zinazofanywa kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.
Ziara hiyo imeongeza msisitizo juu ya umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa dini, taasisi za kijamii na wadau mbalimbali katika kuendeleza huduma za kijamii na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wale wenye mahitaji maalumu.




Maoni yako